Pages

Friday, May 31, 2013

KIKWETE ALIKOROGA MAUAJI YA MWANGOSI :WAHARIRI WAHOJI KUPANDISHWA CHEO KAMUHANDA

 
 

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemvaa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kumpandisha cheo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, badala ya kumchukulia hatua.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kumpandisha cheo Kamuhanda kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) licha ya shutuma kutoka kwa wadau mbalimbali nchini akielezwa kushindwa kuwazuia askari kumuua kikatili mwandishi wa habari wa televisheni ya Chanel Ten, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, katika kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, jana alilieleza gazeti hili mjini hapa jana kuwa uamuzi huo umeonyesha udhaifu mkubwa wa Rais Kikwete.
Alisema Rais Kikwete alipaswa kumchukulia hatua Kamuhanda kufuatia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kumtaja kuwa alikiuka sheria ya vyama vya siasa na kuchangia katika kusababisha mauaji ya Mwangosi.
“Rais Kikwete amefanya hivyo bila kujali kauli iliyotolewa kwa niaba yake na Ikulu kwamba angeeleza hatua yake kuhusu tukio la mauji ya Mwangosi baada ya kupatiwa ripoti ya uchunguzi wa mauji hayo,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema baada ya Rais Kikwete kupatiwa ripoti mbili: ya Kamati ya Jaji mstaafu Ihema, Emmanuel Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu, hajawahi kueleza hatua alizochukua kama ilivyoahidiwa.
“Rais Kikwete kumpandisha cheo Kamuhanda kunaweza kutafsiriwa kuwa ni ‘zawadi’ kwa kazi yake iliyosababisha mauaji, sio tu ya Mwangosi bali yaliyofanywa pia na askari kwa amri yake kwa vijana wa bodaboda mkoani Ruvuma kabla ya kuhamishiwa mkoani Iringa,” alisema.
Alimtaka Rais Kikwete ajitokeze kulieleza taifa vigezo alivyotumia kumpandisha cheo Kamuhanda pamoja na tuhuma zote alizonazo.
Mnyika aliongeza kuwa hatua hiyo ya kumpandisha cheo Kamuhanda na makamanda wengine ambao wamelalamikiwa kuhusu utendaji wao akiwemo Isaya Mungulu na Thobias Andengenye katika matukio mbalimbali ya askari wa chini yao kusababisha mauaji inatoa picha kuwa matendo hayo yalikuwa na baraka ya uongozi wa juu zaidi wa serikali.
“Rais Kikwete kuwapandisha vyeo makamanda hao kumetonesha majonzi ya wote ambao ndugu zao waliuawa kikatili na Jeshi la Polisi, sehemu mbalimbali yakiwemo yale yaliyotokea katika mikutano ya kisiasa,” alisema Mnyika.
Mnyika alisisitiza kuwa Rais Kikwete alipaswa kujitokeza kutoa majibu juu ya barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ya kutaka aunde tume huru ya kijamii kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Kwamba badala yake Jeshi la Polisi ambalo makamanda wake ni watuhumiwa liliachwa lijichunguze ili kulindana na kutoa mwanya wa kuhusika kupanda vyeo badala ya kupanda mahakamani.
Jukwaa la wahariri lashangazwa
Jukwaa la wahariri nchini, limepokea kwa mshangao mkubwa kupandishwa cheo kwa Kamanda Kamuhanda, bila kujali kwamba alisukumiwa lawama na tume mbili zilizoundwa kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Akihojiwa na Tanzania Daima Jumamosi, Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena, alisema inasikitisha kuona serikali ikipuuza vilio na malalamiko ya wananchi kuhusiana na tukio hilo.
“Huyu mtu aliondoka mkoani Ruvuma akikabiliwa na tuhuma za askari wa chini yake kuwaua waandamanaji wa bodaboda na kaja Iringa amekutana na janga lingine.
“Tulitegemea katika utawala wa sheria, hata baada ya kelele za watu wengi na kutia doa kubwa katika utendaji wa polisi, angewajibishwa mara moja,” alisema Meena.
“Sehemu nyingine makamanda wengine walipendwa sana kama Gewe na Tibaigana ambao walifanikiwa kuteka nyoyo za watu kwani walijitahidi kufanya kazi kwa uadilifu.
Katibu huyo alisema waandishi wa habari wanamtazama Kamuhanda kama mtu mwenye kasoro katika utendaji kazi wake, sio tu wakiwa ni waandishi wa habari bali hata raia wa kawaida.
“Hata kama hakuua yeye, lakini kwa matukio haya hasa hili la Mwangosi kwa sababu alikuwepo tangu mwanzo hadi mwisho wa tukio, tulitegemea aondoke na si kupandishwa cheo.
“Kuwepo kwake kumeendelea kutuumiza katika tukio zima; hakuchukua hatua kuzuia hata alipoambiwa. Inaonekana kwao ni utendaji kazi bora kulingana na walivyotaka. Wametusaidia kujua sisi waandishi kuwa tuanze kuitazama serikali kwa jicho la namna gani.
Meena alisema kuwa serikali ingetumia busara kubwa katika jambo hilo, maana tafsiri itakayopokelewa na wananchi ni kwamba serikali ilifurahia mauaji haya, na labda inalea ukatili na mauaji.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga, juzi katika taarifa yake alisema kuwa Rais Kikwete amewapandisha vyeo maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi kuwa Makamishna wa Polisi (CP) na Manaibu Kamishna wa Polisi (DCP).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waliopandishwa kuwa Makamishna wa Polisi ni Isaya Juma Mungulu na Suleiman Kova ambao kabla ya vyeo vyao vipya walikuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.
Isaya Mungulu yuko Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ambapo Suleiman Kova ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Dar es Salaam.
Waliopandishwa kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi ni Elice Mapunda, Brown Lekey, Hamdani Omar Makame, Keneth Kasseke, Abdulrahman Kaniki, Thobias Andengenye, Adrian Magayane, Sospeter Kondela, Simon Sirro na Ernest Mangu.
Wengine ni Hussein Laisseri, Anthony Joel S. Mwami, Mohamed Mpinga, Adolfina Chialo, Mpinga Michael Gyumi, Ally Mlege, Hezron Gyimbi, Michael Kamuhanda, na Jonas Mugendi.
Kabla ya uteuzi huu, maofisa hao walikuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi. Uteuzi huu umeanza mara moja.
 
kwa hisani ya jamii Forum

AFARIKI AKIDANDIA DALADALA

Mtu mmoja ambaye jina lake bado halijafahamika, amefariki dunia baada ya kuteleza na kuanguka wakati alipokua akijaribu kudandia Daladala maeneo ya Ilala Boma, Jijini Dar es Salaam, asubuhi leo. Marehemu huyo baada ya kuanguka na kupiga kichwa kwenye lami, alipasuka kichwa na kuvuja damu nyingi kichwani, na kufariki katika eneo la tukio.





Saturday, May 25, 2013

WATOTO WATANO WAZALIWA SONGEA




Mwalimu Sofia Mgaya akiwa amelala na watoto wake wote watano  kitandani baada ya kujifungua

Na Nathan Mtega,

Songea
 MWANAMKE mmoja mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea mkoani Ruvuma amejifungua watoto watano hai kwa wakati mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji wa uzazi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea.

 Akizungumza Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Dkt.Benedict Ngaiza alimtaja mwanamke huyo aliyejifungua watoto hao watano kuwa ni Sophia Mgaya(28) ambaye ni mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea na kuwa hali za watoto hao zinaendelea vizuri pamoja na kuzaliwa chini ya umri wa kawaida wa kuzaliwa ambao ni miezi tisa.

 Alisema kuwa mama huyo alipokuwa akihudhuria kliniki hospitalini hapo uchunguzi uliokuwa ukionyesha kuwa tumboni mwake kuna watoto wanne ambao walikuwa wakiendelea vizuri tumboni humo lakini mnamo Mei 24 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi alianza kusikia uchungu na kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa upasuaji na kukutwa akiwa na watoto watano hai tumboni mwake.

 Dkt. Ngaiza alisema kuwa watoto watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike na wote wako hai na wamewekwa katika chumba maalumu kwa sababu wamezaliwa wakiwa na umri wa wiki thelathini na nne(miezi nane) na siyo miezi tisa kama ilivyo kawaida.

 Aidha alisema kuwa watoto hao wamezaliwa wakiwa na uzito mdogo huku mwenye uzito mkubwa akiwa gramu 730 na mwenye uzito mdogo akiwa na gramu 430 na huo ukiwa ni uzazi wake wa pili huku mama mzazi wa mwanamke huyo aliwahi kujifungua watoto watatu na wote wako hai na mmoja ni mtoto wa kiume anasomo kidato cha sita katika shule ya wavulana ya Songea.

 
 Alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kutokea katika hospitali hiyo kwa sababu kumekuwepo na matukio ya akina mama kujifungua watoto wawili au watatu na siyo zaidi ya idadi hiyo kama kama ilivyotokea kwa mama huyo 

Friday, May 24, 2013

MWANDISHI NGULI WA NIGERIA CHINUA ACHEBE AZIKWA

 CHINUA ACHEBE ENZI ZA UHAI WAKE


 BAADHI YA WAOMBOLEZAJI WAKIWA WAMEBEBA JENEZA 


BAADHI YA WASHIRIKI KATIKA MAZISHI YA MWANAFASIHI NGULI MAREHEMU CHINUA ACHEBE WAKIWA WAMEVALIA MAVAZI YA KIMILA YA NIGERIA YALIYOFANYIKA JANA KATIKA JIMBO LA ANAMBRA

Melfu ya waombolezaji walijitokeza kwa mazishi ya mwandishi mashuhuri wa nchi hiyo marehemu Chinua Achebe, katika jimbo la Anambra.Wageni mashuhuri akiwemi, rais Goodluck Jonathan pia hawakuachwa nyuma.

Mamia ya watu walikusanyika kanisani baadhi wakivalia mavazi ya kitamaduni yenye picha ya Achebe. Marehemu Achebe alisifika sana kama baba mwanzilishi wa fasihi ya kiingereza barani Afrika.

kwa  hisani ya BBC

Thursday, May 23, 2013

HALI ILIVYOKUA LEO MTWARA











 BAADHI ya wananchi wa eneo la magomeni mkoani Mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo

Kwa sasa inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokua eneo la magomeni ambako mbomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule

RAISI AZINDUA BARABARA YA IRINGA DODOMA NA KUWEKA JIWE LA MSINGI KATA YA MIGOLI

Na







 Iringa
RAISI wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya  Mrisho Kikwete  jana amefanya uzinduzi wa barabara mpya ya Iringa Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 na kuweka jiwe la msingi katika  ya kata ya Migori jimbo la Isimani Mkoani Iringa
Alisema kutokana na kuwa na mahusiano mazuri na wafadhili kutoka nchi za nje ujenzi wa barabara hiyo umewezeshwa na  mikopo kutoka benki ya serikali ya Japan na benki ya maendeleo ya Afrika   pamoja na serikali  ya Tanzania.
Kikwete alisema lengo la serikali ni kuunganisha barabara zote zinazounganisha mikoa zenye kiwango cha chini kua na kiwango cha lami na kwamba  barabara hiyo ni moja ya barabara kuu za Afrika  hivyo kuwepo kwa  barabara hiyo kutainua utalii na kukuza  uchumi  wa mkoa na nchi kwa ujumla
‘’bila shaka serikali imejitahidi kujenga barabara na lengo la serikali ni kuunganisha barabara zote  japokua ujenzi wake ni ghali sana lakini pia kuna manufaa makubwa  na barabara hii tunatarajia kuimaliza mwaka 2015’’
Alisema barabara ya Iringa Dodoma itawasaidia wananchi wa kusini kwenda mikoa ya kaskazini  kwa urahisi ukitofautisha na usumbufu ulikuwepo awali ambapo wananchi walilazimika kipita Chalinze  kwenda mikoa ya Arusha
Pia raisi Kikwete alieleza kuwa barabara  ya Iringa Dodoma itagharimu kiasi cha Tsh Bilioni 232.2 na kwamba kiasi cha shilingi Bilioni 1.9 kilitumika kuwalipa fidia baadhi ya wananchi waliokuwa na makazi ndani ya hifadhi ya barabara hiyo.
Hata  hivyo Jakaya amewaasa wananchi wanaoizunguka barabara hiyo kuacha kurudisha nyuma shughuri za maendeleo kwa kuiba baadhi vitendea kazi vikiwemo vipuli pamoja na mafuta kwani kwa kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao wenyewe.
Mbali na hayo raisi Kikwete amewaasa wananchi kuwa makini na gonjwa hatari la Ukimwi kwani uwepo wa barabara hiyo utaongeza idadi kubwa ya watu hivyo kuchukua tahadhari mapema.
‘’Uwepo wa barabara hii utaongeza wingi wa watu na wingi wa magari hivyo nawaasa kua makini kwa kupalamia wageni hovyo kwasababu barabara hii itatumika na watu tofauti kutoka nchi mbali mbali’’Alisema
Nae waziri wa ujenzi Dk John Magufuli alisema wakandalasi watakaozembea katika shughuri nzima ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo serikali haitawavumilia na badala yake watafukuzwa
Magufuli  amempongeza Mbunge Wa Isimani William Lukuvi kwa uchapa kazi wake na kwamba endapo mbuge huyo angeamua kugombea jimboni kwake basi asingeweza kusimama nae bali angemuachia.

Thursday, May 16, 2013




 Sister Feki Phylis Wanjiru Kamau.

 JESHI la polisi mkoa wa Iringa limemkamata mwanamke Phylis Wanjiru mwenye umri wa miaka 44 aliyevalia mavazi ya kitawa wa masister wa kanisa Kathoriki, ambapo baada ya kupekuliwa amekutwa na baadhi ya vielelezo vilivyobaini kuwa ni tapeli.

Wanjiru ambaye ni raia wa nchi ya Kenya amekamatwa na jeshi la polisi baada ya masister wenzie kubaini kama si mmoja wao, kutokana na kushindwa kufanya baadhi ya masuala  ambayo ni msingi wa utawa wao.

Akizungumzia mkasa huo, kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda amesema mwanamke huyo kabila laKe ni Muwembu wa nchini Kenya amekamatwa katika nyumba  za masista zilizopo Ipogolo mjini Iringa.

Aidha Kamuhanda amesema mwanamke huyo ambaye awali aligoma kutoa maelezo ya kina juu ya ujio wake nchini Tanzania, katika upekuzi walimkuta na baadhi ya chip (Line) za makampuni mbalimbali ya simu ya ndani na nje ya nchi.

Kamuhanda amesema Sister huyo bandia alikutwa pia akiwa na hati za kusafiria (Passport) mbili, moja ikiwa niya Africa Mashariki yenye namba Ke. 020659 huku hati ya nyingine ikiwa na jumuiya ya Kenya namba A. 1790366.

Amesema Sister huyo feki katika hati hizo ilionyesha kuwa alitembelea nchi ya Rwanda, Uganda pamoja na nchini Tanzania ambapo siku za hivi karibuni alikuwa Mkoani Mara Tarime.

Sister huyo FEKI amekuwa akitumia mbinu ya kujiangusha kama mtu mwenye ugonjwa wa kifafa pindi anapofanyiwa mahojiano, jambo linalowawia vigumu jeshi hilo kupata maelezo ya kina dhidi ya dhamira yake ya kuingia humu nchini.

Kamuhanda ameitaka jamii kuwa makini na wageni mbalimbali, huku akiwaasa kuacha tabia ya kuwaamini watu kwa muonekano wao, kutokana na mwanamke huyo kutumia njia hiyo ambayo inamfanya kila mtu kumuamini.