Pages

Wednesday, December 19, 2012

MSANII WA FILAMU JUMA KILOWOKO AANGUKA JUKWAANI ARUSHA


 Msanii wa filamu nchini,Juma Kilowoko akiwa ameshikwa na wasanii wenzake mara baada ya kuanguka jukwaani juzi ndani ya uwanja wa Sheikh Amri katika tamasha la wasanii wa muziki wa kizazi kipya na wale wa filamu


Akipewa pole na wenzake waliomdaka baada ya kuanguka

Msanii wa filamu nchini,Juma Kilowoko akiwa ameshikiliwa na wenzake wakimshusha chini ya jukwaa mara baada ya kuanguka
 alipopewa nafasii ya kuwasalimia mashabiki wake.
 
HALI ya msanii  wa filamu nchini,Juma Said Kilowoko maarufu kama Sajuki imeelezwa si ya kuridhisha  mara baada ya msanii huyo juzi kuanguka jukwaani mara baada ya kuishiwa na nguvu wakati alipopewa kipaza sauti kuwasalimia mashabiki waliofurika kumtizama.

Tukio hilo lilitokea juzi jumapili katika tamasha la wasanii wa filamu na wale wa muziki wa kizazi kipya lililofanyika  ndani ya uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid  wakati msanii huyo alipopandishwa jukwaani kuwasalimia mashabiki wake.

Mara baada ya msanii huyo kupandishwa jukwaani alipewa kipaza sauti ili aweze kuwasalimia mashabiki wake lakini katika hali ya kawaida alifanikiwa kutamka neno moja tu”ahhh” na kisha kudondoka chini ya jukwaa lakini kabla ya kutua chini alidakwa na wasanii waliokuwa pembeni yake.

Hatahivyo,wasanii hao walimkalisha chini ya jukwaa hilo ili aweze kupumzika na kisha baada ya muda mfupi walimshusha chini ya jukwaaa hilo ili aweze kupata muda wa kupumzika zaidi.

Akihojiwa na gazeti hili muda mfupi mara baada ya kushuka jukwaani Sajuki kwa sauti ya upole alisema kwamba hali yake kiafya si nzuri kwa kuwa hana nguvu na anahitaji matibabu zaidi.

”Kaka hali yangu si nzuri kabisa naumwa sana sijisikii vizuri”alisema Sajuki huku akionekana mnyonge zaidi
 Hatahivyo,baadhi ya mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani hapo walionyeshwa kustushwa na hali ya msanii huyo huku wengine wakiwatupia lawama nzito baadhi ya wasanii wa filamu nchini walioambatana na msanii huyo kwa madai kwamba wanamtumia ili wapate pesa ilhali mwenzao ni mgonjwa.

Wakihojiwa kwa nyakati tofauti mashabiki hao kwa jazba walisema kwamba msanii huyo alipaswa kupewa muda mwingi wa kupumzika kuliko kuambatana na wenzake mikoani kwani hali hiyo inamchosha zaidi.

“Hawa watu wa Bongo movie ni watu wa ajabu sana huyu mtu anaumwa sana sisi tunashangaa wanaambatana na mtu mgonjwa mikoani wampe muda apumzike na si kumtumia kwa kupata pesa”alisikika shabiki mmoja akiongea kwa jazba.

Picha na habari kwa hisani ya Full Shangwe Blog
 

 

MTOTO GIFT AUAWA KIKATILI KWA KUCHALANGWA MAPANGA NA BABA YAKE MZAZI

Marehemu Gift Mustafa


Kwenda kuzika


Waombolezaji msibani kwa akina Mustafa


Mama Mzazi wa Gift


Na huyu ndio baba mzazi wa marehemu Gift alieua mtoto wake Bwana Mustafa Mchele


Ni mtoto mdogo lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo ndiyo maana alipowakuta baba na mama yake wanapigana, haraka sana alihoji sababu ya ugomvi wao, akataka waachiane.
Kumbe baba ni katili, eti swali “kwa nini baba unampiga mama”, likamuudhi, hivyo akamcharanga mapanga Gift mpaka akapoteza maisha.

Mtoto Gift, ameuawa kikatili mno, picha za tukio tumeshindwa kuzitumia kutokana na maadili, zinaonesha jinsi muuaji alivyomkatakata usoni na kichwa kizima bila huruma.
Gift, aliuawa Desemba 10, 2012, nyumbani kwao, Yombo Buza, Temeke, Dar es Salaam.

Mama wa marehemu, Zulfa Mustapha na majirani zake, wanamlilia Gift, wakimuelezea alikuwa mtoto mzuri, mwenye akili na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo licha ya umri mdogo aliokuwa nao.
SIKU YA TUKIO
Jirani aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema, Gift alikuwa anatoka madrasa, alipofika nyumbani aliwakuta wazazi wake wanagombana.
“Ni kawaida ya Gift kufuatawa na ama baba yake au mama yake pindi anapokuwa madrasa lakini siku hiyo hakufuatwa, kwa hiyo alifika nyumbani amechelewa kidogo.

“Inaonekana alisubiri kwa muda kabla ya kuamua kurudi mwenyewe. Akakuta wazazi wake wanagombana, hakujua kama amekikaribia kifo chake.
“Mama yake alikuwa analia, kwa hiyo akamuuliza baba yake ni kwa nini alikuwa anampiga mama yake. Hapohapo, baba mtu akachukua panga na kumcharanga.
“Baada ya kumcharanga mtoto, akamgeukia mkewe, akamkata mkononi na kichwani jeraha moja lakini mama mtu yeye alipata upenyo na kukimbia,” alisema jirani huyo.

MAMA ALIPONA
Ripota wetu, walifanikiwa kumuona Zulfa akiwa na majeraha mawili, moja mkononi na lingine kichwani lakini hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Hata hivyo, jitihada za maripota wetu kuzungumza na Zulfa ziligonga mwamba kutokana na ndugu zake kuwa wakali.
Wikiendi iliyopita, maripota wetu walifika nyumbani kwake lakini wakaelezwa kwamba ndugu zake wamemhamishia sehemu nyingine.

MTOTO AZIKWA
Gift, alizikwa Desemba 12, mwaka huu kwenye makaburi ya Yombo Buza, Temeke, Dar es Salaam.
Simanzi ilitanda kwa wakazi wa Yombo, husasan majirani wa familia ya Mustafa Mchele, kwani tukio hilo limekuwa na sura ya aina yake
Majirani wamesema kuwa Mustafa hakutegemewa na jamii kutenda mauaji hayo kutokana na asili yake ya upole na ukarimu kwa watu.
Wamesema kuwa pia ni mtu anayemjua Mungu vilivyo, kwani husali swala tano.
“Ni msomi, alikuwa akiishi na familia yake vizuri. Tuliposikia mauaji haya tumeshangaa sana, wengi wamehisi kuna mambo ya uchawi hapa,” alisema jirani huyo na kuongeza:
“Wengi wanaamini akili ya Mustafa imechezewa. Katika siku za hivi karibuni kila alipokuwa akienda kazini alikuwa akiumwa, akirejea nyumbani huwa mzima.

Jirani mwingine ambaye naye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema: “Mustafa alikuwa anafanya kazi kwenye kiwanda kimoja kilichopo Barabara ya Nyerere lakini siku za karibuni, alikuwa nyumbani mara nyingi kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
“Kule kiwandani ni kiongozi wa wafanyakazi. Kwa nini aumwe akiwa kazini, akifika nyumbani anapona? Mbona si mtu wa ugomvi, sasa ilikuaje agombane na mkewe kisha amuue mtoto wake kipenzi? Kuna kitu hapa!”
Majirani walisema, Mustafa alikuwa anampenda mno Gift na hata siku ya tukio aliongozana naye mpaka madrasa ambako mtoto huyo alikuwa anasoma