NDUGU WA SAMSON DANIEL ALIYOWATEKETEZA KWA MOTO 2010
Mahakama kuu Kanda ya Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 35 Samsoni Daniel Mwang’ombe baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia ndugu wa familia moja wapatao saba.
Akisoma mashtaka mbele ya jaji wa mahakama hiyo Samwel Karua, Mwendesha mashtaka wa Serikali Rhoda Ngole alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 21, 2010 kinyume cha kifungu cha 195 (16) kilichofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.
Ngole aliiambia Mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo mwaka huo majira ya 2:00 hadi saa 2:30 usiku ambapo alifika nyumbani kwa baba yake akiwa na sigala mkononi huku akiivuta na baadaye kuidondosha sigala hiyo iliyosababisha moto kuwasha nyumba.
Aliwataja walioathirika na moto uliokuwa umewashwa kutokana na sigala aliyokuwa ameidondosha mtuhumiwa kuwa ni Daniel Mwang’ombe, Anitha Richard, Salome Mwang’ombe,Jane Samson, Diana Samson, Maria George na Cloud Samson.
Kutokana na kosa hilo mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na kwamba aliua bila kukusudia ambapo alikiri kuwa akiwa anavuta sigala alidondosha kipande hicho ambacho kilikuwa bado kinawaka moto.
Aidha Mwendesha huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa pamoja na mtuhumiwa kukiri kusababisha vifo bila kukusudia mahakama impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Wakili wa upande wa utetezi Sambwee Shitambala alisema Mahakama inatakiwa kumwonea huruma na kumpunguzia adhabu mshtakiwa kutokana nay eye kuwa miongoni mwa wafiwa.
Alisema mshtakiwa ameondokewa na wazazi, watoto na mke katika ajali hiyo ambapo hakuhudhuria mazishi yao pia amekaa muda mrefu akiwa mahabusu ambapo amekaa kwa miaka mitatu na kuongeza kuwa mtuhumiwa ni kijana ambaye ni nguvu kazi ya taifa hivyo hastahili kufungwa.
Na Venance Matinya, Mbeya.