Pages

Wednesday, November 21, 2012

VIJANA WA UMRI KATI 20 NA 45 KUTOJITOKEZA KUPATA HUDUMA YA TOHARA

Na Mercy Mwalusamba

Iringa

Huduma ya tohara inayoendelea kutolewa katika hospitali ya mkoa  wa Iringa imekuwa na mafanikio katika kipindi cha mwaka 2010 – 2011 kufuatia kampeni maalumu ya dondosha mkono sweta


Akizungumza na waandishi wa habari jana Muuguzi wa hospitali ya Mkoa katika kitengo cha upasuaji Iluminata Sanga alisema kabla ya mpango wa serikali juu ya huduma ya tohara na uhamasishaji katika  kampeni ya dondosha mkono sweta,  hali ya wananchi waliopata huduma hiyo ilikua chini kwa asilimia 35


Alisema baada ya mpango mkakati kuanza mwaka 2010 huduma imetolewa kwa mpango maalumu kupitia hospitali ya mkoa pamoja na vituo vya afya vya Ngome manispaa,hospitali ya Tosamaganga  Mufindi na Lugoda ambapo jumla ya watu waliopata huduma ni 10,302 hadi sasa


Huduma ya tohara imefanyika kwa kiwango kikubwa vijijini ikilinganishwa na mjini ambapo wengi wao ni watoto kati ya umri 10 hadi 14 na 15 hadi 20  idadi iliyofikia asilimia 65 alisema Sanga

Sanga alisema hali ya usafi kwa mtu aliefanyiwa tohara ndio jambo la msingi kwani bila kua na hali ya usafi katika kidonda husababisha madhara na kidonda kutokupona haraka

“Watu wanaokuja kupata huduma wamekuwa wakipewa elimu ya ushauri nasaha na upimaji wa afya kwakuzingatia vipimo muhimu ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea baada ya tohara” alisema

 
Aliongeza kuwa kumekuwa na baadhi ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 ambao hufika peke yao kupata huduma hii bila wazazi wao au walezi kinyume na utaratibu kwani huduma kwa watoto wa umri huo  hutolewa chini ya uangalizi na usimamizi wa wazazi

Alisema kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na  tohara ili kuepukana na changamoto zilizojitokeza kama kufikiri kufanyiwa tohara ni kuruhusu kuendelea kufanya vitendo vya ngono au kupunguza nguvu za kiume

“tohara inamsaidia mtu kuishi katika mazingira salama ya kupunguza uwezekano wa maabukizi ya magonjwa ya ngono”


……………………….MWISHO……………………..



MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI AFIKISHWA MAHAKAMANI TENA

Na mercy Mwalusamba

Iringa
 
MTUHUMIWA wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi alifikishwa mahakamani jana katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari wakiendelea kuzuiwa na polisi kupiga picha.

Askari wa kikosi cha kuzuia ghasia wengine waliokuwa na silaha mbalimbali huku wengine wakivaa kiraia waliweka ulinzi mkali kuhakikisha waandishi wa habari hawapati mwanya wa kupiga picha.

Mwendesha mashtaka wa serikali Adolf Maganda aliambia mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dyness Lyimo kuwa upelelezia wa kesi hiyo haujakamilia.

Pasificus Cleophace Simon (23) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa tuhuma ya kumuua kwa makusudi mwandishi huyo katika ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa uliofanyika Septemba 2 mwaka huu.

Mtuhumiwa huyo mwenye namba G 2573 alifikishwa mahakamani hapo kwa
gari la polisi lenye namba PT 1404 likiwa na ulinzi mkali akiwa amefichwa uso kiasi cha kutoonekana macho yake.

Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari lenye namba za kiraia T 320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO huku kwa mara ya pili akifikishwa kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pick up akiwa katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari wakidhibitiwa na polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililozusha hisia tofauti miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.

Kwa mujibu wa wakili huyo, upelelezi haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Desemba 05 mwaka huu itakapotajwa tena.

Unyanyaswaji wa waandishi wa habari wakati wa kupiga picha za mtuhumiwa wa mauaji hayo unaendelea kushika kasi baada ya mwandishi wa gazeti Tanzania daima kupigwa na askari kanzu kwenye chumba cha mahakama alipotaka kupiga picha kabla ya mahakama kuanza jambo ambalo limelaaniwa vikali na waandishi pamoja na wananchi waliokuwepo mahakamani hapo.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 mwaka huu katika kijiji cha Nyololo yo alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguzi wa matawi hayo.
 
………………………………………………. Mwisho ………………………………………..