Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard
( wa nne kushoto mwenye begi ndogo begani) akiwa nje ya mahakama kuu
kanda ya Iringa na wanahabari wengine mara baada ya kesi ya mtuhumiwa wa
mauaji ya Daudi Mwangnosi kusikilizwa
Waandishi wakisubiri kupiga picha ya mtuhumiwa bila mafanikio hadi wanaondoka eneo la tukio (mahakamani)
KESI
ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Mkoani Iringa, Daudi
Mwangosi imeanza kusikilizwa hii leo baada ya kilichoelezwa na upande wa mashtaka
kwamba uchunguzi wake umakamilika.
Kama
ilivyo ada, makechero wa Polisi wengi wao wakiwa wamavaa kiraia walikuwepo
mahakamani hapa huku wakijaribu kuwazuia wanahabari kutekeleza wajibu wao.
Katika
mazingira ya kutatanisha, mwandishi wa habari wa gazeti la Habarileo, Frank
Leonard ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa
alikamatwa na askari wanne waliokuwa wamevaa kiraia kwa kile kilichoelezwa
kwamba alikuwa akipiga picha mahakamani wakati kesi ikiendele
Baada
ya kukamatwa Leonard, alifikishwa kituo cha Polisi cha Kati mjini Iringa na
kuachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuachiwa huru, Leonard alisema "wapo
baadhi ya askari kwa makusudi wanataka kubomoa mahusiano baina ya wanahabari na
jeshi la Polisi ambayo yanaendelea kujengwa na kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Iringa, Ramadhani Mungi."
Alisema
kitendo cha kubambikiziwa tuhuma ndani ya muhimili wa dola unaojitegemea
(mahakama) ni kitendo cha uzalilishaji kinachotaka kuaminisha umma kwamba
wanahabari ni watu wasiotaka kufuata taratibu za kimahakama.
Alisema akiwa ndani ya chumba cha mahakama hiyo alikamatwa na askari hao bila
idhini ya Jaji wa Mahakama Kuu wakati akizima simu yake ya mkononi iliyokuwa
katika mtetemo.
"Nilikuwa nazima simu yangu hao askari hao kwasababu wanazojua wao wenyewe
waligeuza suala hilo ili lionekane katika sura wanayoitaka na hatimaye
wanifungulie mashtaka," alisema.
Alimshukuru
Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Iringa, Ngoi kwa kumtendea haki na baada ya
kupata ushahidi kufutilia mbali kesi hiyo.
Akizungumza na wanahabari, Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa, Dunstan Nduguru aliwashangaa Polisi kwa kuingia shughuli za mahakama.
"Hata
kama mwandishi huyo angekuwa anapiga picha, haikuwa kazi yao kumkamata mpaka
wapewe agizo na Jaji Mfawidhi aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo," alisema.
Pamoja
na askari hao kuwazuia wanahabari kuchukua picha mara baada ya mtuhumiwa huyo
kufikishwa mahakamani, Nduguru alisema utaratibu wa mahakama unawaruhusu
wanahabari kuchukua picha kabla shughuli kabla shughuli za mahakama hazijaanza
na baada ya shughuli hizo kwisha.
"Kuwazuia
wanahabari kufanya kazi zao kwa utaratibu huo sio sahihi; siku nyingine mkiona
kuna dalili ya kupata bugudha kama hiyo naomba mnijulishe ili niondoe mzozo
huo," alisema.
Mbele
ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa, Mary Shangali,
Wakili wa upande wa mashtka, Adolph Maganga alisema Adolph Maganda alisema kwa
kukusudia mtuhumiwa Pacificius Cleophace Simoni anatuhumiwa kumuua Mwangosi
kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura ya 16
kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Alisema katika tukio hilo lililotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa, mshtakiwa alifyatua bunduki yake na kusababisha kifo cha marehemu, papo hapo.
Alisema
siku ya tukio marehemu alikuwa Nyororo kwa ajili ya kuripoti na kutoa taarifa
kwa umma juu ya mkutano uliokuwa ufanywe na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
Alisema mshtakiwa akiwa mmoja wa wafanyakazi wa Polisi, waliwasihi Chadema wasifanye mkutano huo kabla wafuasi wake hawajaanza kurusha mawe kwa Polisi na baadhi yao kupata majeraha.
Kutokana
na mzozo huo, wakili huyo wa serikali alisema polisi walipiga mabomu ya machozi
ili kuwatawanya wafuasi hao kabla mshtakiwa huyo hajamfyatulia bomu marehemu.
Wakili
huyo aliwasilisha ramani ya eneo la tukio, ripoti ya mtaalamu wa milipuko na
ripoti ya daktari aliyechunguza mwili wa marehemu Mwangosi na gazeti la Mwananchi
la Septemba 3, 2012 lililochapisha picha ya tukio hilo katika
ukurasa wa mbele kama vielelezo vinavyohusiana na kesi hiyo.
Wakili
wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage alitaja mambo wanayokubaliana katika kesi
hiyo kuwa ni jina na anuani ya mshtakiwa na kwamba marehemu Mwangosi alikufa
kifo ambacho si cha kawaida.
Na
kwamba mshtakiwa Simoni alikamatwa na amefikishwa mahakamani akihusishwa na
mauaji hayo.
Wakili
Kaijage alisema vielelezo vingine vilivyoletwa na upande wa mashtaka
hawakubaliani navyo kwakuwa vinahitaji ushahidi kutoka kwa wahusika.
Jaji
Shangali aliahirisha kesi hiyo mpaka kikao kingine cha mahakama kuu
kitakapoitwa ili ianze kusikilizwa.