Mtoto wa miaka minne (jina limehifadhiwa), amedhulumiwa haki yake ya utu
na kuteswa kwa zaidi ya miaka mitatu, kwa kufungiwa ndani ya boksi kama
mnyama, ili asimuambukize mama mlezi virusi vinavyosababisha Ukimwi.
Unyama huo wa kusikitisha, umefanyika muda wote huo kwa mtoto huyo
Morogoro mjini katika mtaa wa Azimio bila kuripotiwa popote, huku wakazi
na majirani wa nyumba hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba
yake mzazi akiendelea na maisha kwa kumuogopa mkewe.
Wakizungumza na mwandishi jana, majirani hao walidai Mariam alihamia
katika nyumba hiyo mwaka 2010, lakini hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto.
Hata hivyo majirani hao walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto
akikohoa na kulia hasa nyakati za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi
kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga watu waliouawa
kishirikina au kwa jina lingine misukule.
Hatimaye juzi mateso ya mtoto huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja
kupata taarifa sahihi, kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na
hatia aliye katika mateso na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo.
Zongo akiwa katika kazi za kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa
kutoka kwa majirani kuwa kuna mwanamke, Mariam Said, amemficha mtoto
ndani ya boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje.
Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti
wa mtaa huo, Tatu Mgagalana na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo
ambapo walimkuta mtuhumiwa, Mariam na kuanza kumhoji kuhusu tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa Zongo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku
akibabaika, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa hali
iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa Mariam kwa nguvu,
hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka
mitatu.
Ofisa huyo na mwenyeji wake walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu
uliotokana na kinyesi na mkojo, kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba
chake cha kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja
ndogo na kubwa.
Hali ya mtoto huyo ilisababisha mashuhuda waliokuwa wamezunguka nyumba
hiyo, kuanza kumshambulia Mariam kwa fimbo na mawe, na kumlazimu Zongo
na mwenyeji wake kufanya kazi ya ziada kumnusuru mtuhumiwa kwa kutoa
taarifa Polisi, huku wakijaribu kuzuia asidhurike.
Baada ya muda askari Polisi walifika na kumchukua mtuhumiwa na alipofika
kituoni, inadaiwa alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na miezi
tisa baada ya mama yake, kufariki dunia mwaka 2010.
Mtuhumiwa huyo alidai Polisi kuwa kwa mara ya mwisho, alimuogesha mtoto
huyo Julai mwaka jana, na alikuwa akimwekea chakula na maji ndani ya
boksi hilo.
Mume wa mtuhumiwa huyo, Mtonga Ramadhani ambaye ni mfanyabiashara wa
Soko la Mawenzi katika Manispaa ya Morogoro naye alikamatwa na katika
mahojiano, alidai hakuona sababu ya kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto
huyo kwa sababu hamhusu na wajibu wake ilikuwa kutafuta chakula tu.
Kwa sasa mtuhumiwa huyo yupo Kituo Kikuu cha Polisi mjini Morogoro na mtoto amepelekwa katika Ofisi ya Idara ya Ustawi wa Jamii.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi ambaye ni mtumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alidai baada ya mzazi mwenzake
kufariki dunia, alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari
alishakuwa na mke.
Alidai kwa kuwa alikuwa ameoa, alikubaliana na upande wa pili wa familia
ya marehemu, kuwa mwanawe huyo alelewe na mama yake mkubwa, Mariam.
Akizungumzia ulemavu wa mtoto huyo, Ofisa Ustawi wa Jamii, Oswin
Ngungamtitu alisema ulemavu huo huenda umetokana na kuishi kwenye boksi
tangu akiwa na miezi tisa hadi sasa bila kutolewa nje, kufanyiwa usafi
wala kupewa chanjo mbalimbali ikiwemo ya polio.
Ngungamtitu alisema ulemavu huo pia huenda umetokana na kukosa lishe
yakiwemo maziwa ya mama, hewa safi na upendo na kwamba mtoto huyo
atakuwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo minyoo, nimonia, utapiamlo na
malaria.
Kutokana na hali hiyo, Ngungamtitu alisema ofisi yake imempeleka katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ili akafanyiwe uchunguzi na
kupewa chanjo ya kutibu magonjwa yatakayobainika.
Baada ya hapo kwa mujibu wa Ofisa huyo, mtoto huyo atapelekwa kwenye
kituo cha kulelea watoto yatima na ikibidi atakabidhiwa kwa baba yake
mzazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo,
mwanamke huyo pamoja na mumewe wanashikiliwa Polisi kwa kosa la
kumfanyia ukatili mtoto kinyume cha Sheria ya Mtoto ya
VIA HABARI LEO