Pages

Thursday, June 6, 2013

AKAMATWA MSIKITINI AKITAKA KUMTAPELI IMAMU NA WAUMINI IRINGA


 Kijana Wiliam Daud a.k.a  Hassan Idd Lumbanga (jina la  kutapeli) mkazi  wa Majengo mkoani Katavi akiwa chini ya ulinzi ndani ya msikiti wa Ijumaa -Miyomboni mjini Iringa baada ya  kushitukiwa kuwa ni tapeli aliyetaka kumtapeli Imamu  wa msikiti  huo wa waumini  wake  leo 


Waumini  hao wakifanya mawasiliano na polisi baada  huku tapeli huyo  kulia akiwa katika hofu kubwa 

 Naibu imamu wa masikiti wa Ijumaa - Miyomboni Issa Boki ( kushoto) akiongozana na  baadhi ya  waumini wa msikiti  huo kumweka  chini ya ulinzi tapeli  huyo (katikati mwenye shati la kijani ambae alitaka  kutapeli kiasi cha  Tsh 55,200 zilizochangwa na  waumini kwa ajili ya kijana  huyo kabla ya  kubaini kuwa ni tapeli  hapa  wakimpeleka  polisi 


 Huyu  ndie  Kijana Wiliam Daud a.k.a  Hassan Idd Lumbanga (jina la  kutapeli) mkazi  wa Majengo mkoani Katavi  aliyeingia msikitini  kufanya utapeli leo

  Kijana Wiliam Daud a.k.a  Hassan Idd Lumbanga (jina la  kutapeli) mkazi  wa Majengo mkoani Katavi  akiwa  chini ya ulinzi ,kulia ni katibu wa msikiti huo Juma Kibasila aliyeshika  kichwa 

 

Kijana  huyo tapeli  akipelekwa  polisi  na  waumini wa msikiti wa Ijumaa -Miyomboni leo  kushoto ni katibu wa msikiti  huo Juma Kibasila 


Waumini  wa  dini ya kiislamu katika msikiti  wa Ijumaa - Miyomboni mjini Iringa  wakimfikisha  polisi  kijana aliyevaa shati la kijani baada ya  kuingia ndani ya msikiti kwa  lengo la kufanya utapeli 

-----------------------------------------------

IKIWA ni siku chache zimepita  toka  kuumbuliwa kwa tapeli mzee aliyekuwa akijifanya hana mikono katika  eneo ya Mikyomboni mjini Iringa ,wimbi la utapeli  laendelea  kutikisha  mkoa  wa Iringa baada ya  matapeli hao  kuja na mbinu mpya  ya  kuingia katika nyumba za ibada na kuwatapeli  waumini .

Mbinu  hiyo  imebainika  leo katika msikiti  wa Ijumaa - Miyombini baada ya  waumini  wa msikiti  huo  kumnasa  kijana Wiliam Daud mkazi  wa Majengo mkoani Katavi ambae amekuwa akifanya kazi ya  utapeli katika misikiti mbali mbali hapa nchini kwa  kutumia jina la    Hassan Idd Lumbanga (jina la  kutapeli) ambalo amekuwa akilitumia misikitini pekee.

Kama  ilivyo ada  siku  zote za mwizi ni arobaini basi  hivi ndivyo ilivyokuwa  kwa kijana  huyo baada ya jana  kufika katika msikiti  huo na  kuungana na  waumini  wake katika swala na  wakati  shughuli  hizo za swala  zikiwa katikati kwa naibu imamu  wa msikiti  huo Issa Boki akiendelea  kuongoza  waumini hao ghafla  kijana  huyo tapeli alijiangusha  chini mfano wa mtu aliyezidiwa na kupoteza fahamu .

Hali  hiyo  iliwalazimu  waumini hao  kusitisha shughuli za ibada na  kutafuta  gari haraka haraka na kumkimbiza  katika Hospitali ya mkoa  kijana  huyo tapeli .

Alisema naibu  imamu  huyo Issa Boki alipozungumza na mtandao  huu  wa www.matukiodaima.com  kuwa baada ya  kufika Hospitali ya  Rufaa ya mkoa  wa Iringa kijana  huyo alitakiwa kulazwa kutokana na  kuonyesha  kuzidiwa  zaidi.

Hata  hivyo  baada ya  wao  kuondoka  Hospitali hapo na kijana  huyo  kupelekwa wodini  kulazwa inadaiwa alionekana ni mtu kama mwenye utindio wa ubongo kutokana na vurugu alivyokuwa akiwafanyia  wagonjwa  wenzake kiasi  cha kuhamishwa na kupelekwa katika wodi  la vichaa ambako pia alifanya vurugu kubwa  na kufanikiwa  kutoroka wodini hapo.

Alisema  kuwa katika hali  ya  kushangaza ni pale tapeli  huyo aliporudi tena msikitini hapo leo na  kuungana na  waumini hao katika swala ya mchana  wa  leo na  kuwaomba  waumini  hao  kumsaidia fedha  ili kurejea kwao Katavi .

Kutokana na maombi hayo  Naibu Imamu  huyo aliwaomba  waumini  wake  kumchangia  fedha  na  kupatikana kiasi cha Tsh 55,200 na  wakati  wakijiandaa kumkabidhi  fedha  hizo mmoja kati ya  waumini aliweza kumtambua  kijana  huyo  kuwa ni tapeli ambae amekuwa akitumia mbinu  hizo na kwa mara ya mwisho  alikuwa jijini Dar es Salaam katika msikiti mmoja na kunusurika  kichapo kwa utapeli  huo wa kujiangusha na baada ya siku moja kurejea  kuomba  fedha ili arejee kwao.

Katibu  wa Msitiki  huo Juma Kibasila alisema  kuwa fedha  hizo hawajaweza kumkabidhi tapeli huyo baada ya kumhoji na  kukiri  kuwa si mgonjwa ila amekuwa akiendesha maisha yake kwa  kutapeli  katika  nyumba  mbali mbali za ibada kwa  kutumia mbinu  hiyo ya kujiangusha kama mgonjwa .

Kibasila alisema  kuwa  kwa ujumla  waumini  wa dini  ya Kiislamu ni  watu  wa  kujitolea kwa watu wenye shida na kuwa iwapo kijana  huyo angefika na kuomba msaada kama msaada  bila  kutumia mbinu ya utapeli kama  hiyo hakukuwa na tatizo ila kutokana na utapeli huo  wamelazimika  kumfikisha  polisi  kutokana na kudai kuwa ana miliki funguo malaya  zinazofungua milango mbali mbali ya nyumba na magari hivyo wanahisi ni mtu hatari zaidi .

Kijana  huyo baada ya  kuhojiwa na mtandao  huu alikiri  kuwa ni tapeli anayetafuta maisha kwa mbinu hiyo na  kuwa amefanya utapeli  huo katika misitiki ,makanisa na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya  watu wengi na kusaidia na  kuwa  kila anapofanya utapeli kama  huo huwa hakosi kiasi kati ya Tsh 50,000 hadi 500,000 kwa tukio  moja .

Hata  hivyo  alisema katika Misitiki amekuwa akitumia jina  hilo la Hassan Idd Lumbanga ila anapokwenda makanisani amekuwa akitumia jina la Wiliam Daud .
VIA/www.matukiodaima.com

RUSHWA YA NGONO YAMUWEKA PABAYA





Na Mwandishi Wetu
MWANAMUME aitwaye Andrew Kabula (34), mkazi wa Kimara Mwisho jijini, hivi karibuni alinaswa gesti akiwa na mwanafunzi ‘denti’ aliyetaka kufanya naye ngono ili ampatie kazi bandarini, Amani lina mkanda kamili.


Kabula a.k.a Afisa Feki alijitapa kwa denti huyo kwamba ni Afisa wa Mamlaka ya Bandari jijini Dar na ana uwezo wa kumpatia kazi kama atampa rushwa ya ngono.
Kwa kutambua kwamba kitendo hicho ni kosa kisheria, denti huyo (jina lake kapuni) aliwasiliana na Oparesheni Fichua Maovu ya Global Publishers ili kumnasa afisa huyo feki.


POLISI WASHIRIKISHWA Waandishi wetu waliwasiliana na polisi wa Kituo cha Mbezi Luis jijini Dar na kumwekea mtego jamaa huyo katika gesti aliyoichagua, iliyopo maeneo ya Kimara jijini Dar.
Afisa huyo kila mara alikuwa akiwasiliana na denti huku akimsisitiza kutoondoka hapo kama kweli alitaka ajira.
Waandishi, askari na denti walitangulia katika gesti hiyo na afisa akataarifiwa na denti kwamba ameshafika eneo la tukio. Yakafuata maelekezo ya kuchukua chumba kutoka kwa afisa huyo aliyedai kwamba yupo mbali kidogo.


ANASWA Saa moja usiku, afisa feki alifika katika eneo la tukio na kuingia chumbani katika gesti hiyo (jina tunalo), huku askari na mapaparazi wakifuatilia nyendo zake.
Bila ya kushtuka kama amewekewa mtego, moja kwa moja afisa aliingia chumbani na kumkuta denti huyo ambaye alizidi kumsisitizia lengo lake.
Baada ya kuhakikishiwa kile anachokitaka na denti huyo, afisa alisaula viwalo vyake vyote na kuwa tayari kwa tendo.
Denti aliendelea kujibaraguza na kutuma taarifa kwa askari na mapaparazi wetu kwamba jamaa alikuwa tayari kwa tendo ndipo timu nzima ikavamia chumbani.


AKUTWA NA VITHIBITISHO Mara baada ya askari kumkamata na kumuweka chini ya ulinzi, afisa huyo alipekuliwa katika simu yake ya kiganjani na kukutwa na meseji kadhaa zikionesha kwamba alikuwa akifanya mawasiliano na wasichana wengi kwa ajili ya kuwapa kazi bandarini.

KUMBE NI TAPELI MZOEFU Katika kudhihirisha kuwa ni tapeli mzoefu, siku hiyohiyo  afisa huyo alikuwa na ahadi na msichana mwingine ambaye katika simu jina lake ‘liliseviwa’ kwa jina la Mariam ili apewe rushwa ya ngono.
Inadaiwa kwamba, tapeli huyo amekuwa akiwadhalilisha wasichana wengi kwa staili yake hiyo ya kuwadanganya kuwapatia kazi na kisha kuwaacha bila ya ajira.


UKWELI HUU HAPA Baada kutiwa nguvuni na kupelekwa Kituo cha Polisi, ilibainika kwamba jamaa si mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari bali ni deiwaka wa udereva wa daladala zinazofanya safari zake kati ya Ubungo na Msata mkoani Pwani.

ATAKA SELO YA PEKE YAKE Katika kuonesha jamaa ni mtata, alipofikishwa kituoni na baada ya kuandikisha maelezo alisema kwamba alikuwa akihitaji selo ya peke yake kwani hataki kuchanganyika na watu.

TAHADHARI YA MHARIRI
Tahadhari inatolewa kwa wasichana, wanatakiwa kuwa makini na kutotegemea njia za mkato katika kufanikiwa, wasipoangalia wataangukia katika mikono ya matapeli wa ngono- Mhariri.


hisani ya GPL