"HATA BURE HATUZITAKI"
Shughuli za biashara ya maduka na huduma mbalimbali za kijamii katika jiji la Mwanza zimesimama kwa siku nzima kufuatia mgomo wa wafanyabiashara wakubwa na wa kati zaidi ya 2000, wanaopinga matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki-EFD .
Ni sauti za wafanyabiashara wa jiji la Mwanza, wakiwa wamekusanyika katika kituo kikuu cha zamani cha mabasi cha stendi ya Tanganyika,
kilichopo katikati ya jiji la Mwanza, huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe unaoelezea namna wanavyonyanyasika kutokana na matumizi ya mashine hizo
Baadhi ya wafanyabiashara wakizungumza kwa jazba, wamesema hawako tayari kufanya biashara kwa kutumia mashine za TRA, hata kama watapewa bure kwa madai kwamba wengi wao bado ni wajasiriamali ambao mitaji yao bado ni midogo, huku wengine wakidai kwamba TRA haijawapa elimu kuhusu matumizi ya mashine hizo zaidi ya kuwapa muda wa kuanza kuzitumia
Mgomo huo, ambao umeathiri maelfu ya wakazi wa jiji la Mwanza na kusababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa, wanaotegemea kununua bidhaa mbalimbali kutoka katika maduka ya jumla yaliyopo jijini Mwanza, umemlazimu meneja wa mamlaka ya mapato ( TRA ) mkoa wa Mwanza Bw. Jeremiah Lusana pamoja na kaimu katibu tawala wa mkoa wa Mwanza Bw. Ndaro Kulwijila kuutolea tamko.