Pages

Tuesday, December 10, 2013

WOSIA WA MANDELA WAZUA MJADALA MZITO....!!


Marehemu Nelson Mandela enzi za uhai wake.
Mwandishi Wetu na Mitandao
WOSIA aliowahi kuuandika hayati Nelson Rolihlahla Mandela ‘Mzee Madiba’ au ‘Tata’ (95) enzi za uhai wake akielezea anavyotaka azikwe, ndiyo tishio kubwa lenye utata kuelekea siku ya mazishi yake, Jumapili ijayo, Ijumaa Wikienda limebaini.
Mtandao mmoja nchini humo umeukumbushia wosia huo huku familia ikianza kuonesha misimamo tofautitofauti, hali inayoashiria kuibuka kwa makundi mawili yanayokinzana.

Gari lililobeba mwili wa Nelson Mandela.
FAMILIA INAVYOTAKA
Habari za ndani zilisema kuwa familia inataka mazishi ya kiongozi huyo maarufu duniani yawe makubwa na ya kisasa kwa vile viongozi wa nchi mbalimbali duniani watahudhuria.
“Mandela ni kingozi mkubwa sana duniani, mazishi yake lazima yawe makubwa pia ya kisasa. Hawezi kuzikwa kama mwananchi wa kawaida,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Mmoja wa waombolezaji akigusa picha na Mandela.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa wakati familia hasa wajukuu na watoto wake wakishikilia msimamo huo, wapo wanandugu wanaotaka azikwe kama alivyoandika katika wosia wake huo.
SERIKALI YAPANGA MAMBO BILA KUFUATA WOSIA
Habari zaidi zilisema kuwa Serikali ya Afrika Kusini inajitahidi kuupangua wosia huo kwa kuendelea na maandalizi ya mazishi kama haukuwahi kuwepo licha ya kwamba jamii ya watu nchini humo inaheshimu wosia wa marehemu.
WOSIA UNAVYOSEMA
Mzee Madiba alishauandika wosia huo kwenye karatasi moja tu ambapo aliagiza anavyotaka azikwe. Alisema kuwa akifa azikwe katika milima iliyojitenga nyumbani kwa mababu zake katika Kijiji cha Qunu, Eastern Cape huko ‘Sauzi’.


Waombolezaji wakiweka maua katika sanamu la Mandela.
ALITAKA MAZISHI YA KAWAIDA SANA
Inadaiwa wosia huo aliuandika Januari, 1996 wakati bado akiwa rais ambao ulijaa maelekezo yote juu ya mazishi yake. Aliagiza kufanyiwa mazishi ya kawaida sana yenye hadhi ya raia wa kawaida nchini humo hivyo kuyafanya kuwa makubwa na ya kifahari ni kukiuka wosia wa mzee.
KABURI ALILOLITAKA MANDELA
Katika wosia wake huo uliotolewa na rafiki yake wa karibu, Mzee Madiba aliandika kuwa akifa azikwe katika eneo la familia lenye makaburi ya ukoo wa Mandela kijijini hapo.
Pia aliagiza kuwa kaburi lake liwekewe jiwe la kawaida kama alama ya mahali lilipo ili lisije kupotea kwa mvua au mabadiliko ya tabia nchi.


Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
KABURI LISISAKAFIWE
Katika tafsiri ya maneno hayo, Mzee Madiba alitaka kaburi lake liwe la kawaida sana, akimaanisha lisijengewe kama ilivyokuwa kwa makaburi ya viongozi wengine wa mfano wake barani Afrika kama, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Kamuzu Banda (aliyekuwa Rais wa Malawi).
WOSIA WAKE ULIKUWA WA UPANDE MMOJA WA KARATASI
Magazeti ya nchini humo, South African Mail na Guardian miezi ya karibuni yaliripoti kumnukuu rafiki huyo wa siku nyingi wa familia ya Mandela akisema: “Madiba hakuwahi kukifanya kifo kuwa jambo kubwa la kufikiriwa, pia hakuwahi kutaka chochote cha fahari wakati wa kumzika.” 
Cha ajabu, wosia huo wa Mandela ulitosha kwenye upande mmoja wa karatasi ya kawaida ya kuandikia licha ya kwamba mauzo ya kitabu chake cha Long Walk to Freedom na michoro yenye jina lake vilimpatia mamilioni ya fedha.


elson Mandela (kulia) akiwa na Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wao.
FAMILIA YACHUKIZWA NA WOSIA
Wosia huo ulielezwa kuwashangaza watu wengi duniani kwani waliamini angekuwa na vitu vingi vya kuandika kulingana na uwezo wake.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini, SABC, suala hilo la sehemu atakayozikwa Mzee Madiba liliiudhi mno familia yake akiwemo yule mjukuu wake ambaye ni chifu, Mandla Mandela aliyewahi kufikishwa kortini kwa kuhamisha makaburi hayo ya ukoo na kuyapeleka sehemu nyingine. Pia ndiye msemaji wa familia ya Mandela.
DUNIA YAMKATALIA
Baadhi ya wanaharakati ulimwenguni kote walisema wosia huo unapingana na matakwa ya dunia nzima, ambapo walitaka maziko ya mzee huyo yawe  makubwa na ya kihistoria ambayo hayajawahi kutokea.Ilifahamika kwamba dunia inataka mazishi hayo yavunje ile rekodi iliyoshikiliwa na mazishi ya Papa John Paul II aliyefariki dunia Aprili 2, 2005.


Mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela.
SAFARI HII HAKUKIMBIZWA HOSPITALI
Mzee Madiba ambaye alitimiza umri wa miaka 95 Julai 18, mwaka huu, alikuwa hospitalini kwa karibu miezi  mitatu nyuma akitibiwa maambukizi kwenye mapafu huku akipumulia mashine. Baadaye alipata nafuu na kurudishwa nyumbani ambako usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita aliugua ghafla na kufariki dunia.