MIAKA miwili imepita tangu Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Frank Moshi alipo andika hukumu iliyomwachia huru aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC1), Jerry Murro na wenzake wawili,Edmund Kapama maarufu kama ‘Dokta’ na Deogratius Mugassa.
Katika Hukumu Hakimu Moshi akisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washitakiwa bila kuacha mashaka yoyote,hata hivyo upande wa Jamhuri ilikata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.
Rufaa hiyo inatarajiwa kuendelea kuunguruma tena kesho Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya mrufani (Jamhuri) ya kutaka Muro na wenzake warudishwe kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili kesi yao ianze upya kusikilizwa.
Maombi hayo yalitolewa na Mawakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya na Awamu Mbagwa, Februari 18, mwaka huu, siku ya kwanza ya usikilizwajiwa rufaa hiyo ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyowaachia huru Muro na wenzake. Hatahivyo Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilitupilia maombi hayo ya Jamhuri na badala yake iliamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.
Katika rufa hiyo kesho upande wa Jamhuri itaendelea na hoja zake nyingine za kupinga hukumu ya Kisutu, ingawa Wakati wakitupilia mbali maombi hayo ya Jamhuri, Jaji Dk Fauz Twaib hakutoa sababu za kutupilia mbali maombi hayo ya Jamhuri na kudai kwamba atatoa sababu zake kwenye hukumu ya rufaa hiyo.
Katika maombi yake Jamhuri ilidai kuwa mwenendo wa kesi ya msingi una makosa ya kisheria, kwa kuwa Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo (Gabrile Mirumbe), alikosea kuweka kumbukumbu za mwenendo huo.
Wakili Mbagwa alidai kuwa kutokana na kasoro hizo, hata Hakimu (Frank Moshi) aliyeandika hukumu aliegemea katika mwenendo huo ambao haukurekeodiwa vizuri namatokeo yake hata hukumu aliyoitoa si sahihi .
Alifafanua kuwa kuna ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka umerekodiwa kwa namna ambayo hauakisi uhalisia wa kile kilichozungumzwa, na kwamba baadhi ya sehemu za ushahidi hazikurekodiwa kabisa.
Hata hivyo Mawakili wa wajibu rufani, Richard Rweyongeza naMajura Magafu walidai kuwa hoja za mrufani (Jamhuri) haziko wazi na kwamba hata kama kasoro zinazolalamikiwa zipo,lakini mrufani hajaonesha yalivyoathiri hukumu.
Wakili Magafu alidai kuwa kitendo cha Jamhuri kuomba kesi hiyo isikilizwe upya ni sawa na biashara ya kuchagua mahakimu kwamba wakishindwa kwa hakimu mmoja wanakwenda kubahatisha kwa hakimu mwingine.
Muro na wenzake, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni, kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari 5, mwaka 2010, na kusomewa mashtaka ya kula njama na kuomba rushwa kutoka kwa Wage.
kwa hisani ya habarimpya
No comments:
Post a Comment