Mwalimu Sofia Mgaya akiwa amelala na watoto wake wote watano kitandani baada ya kujifungua
Na Nathan Mtega,
Songea
MWANAMKE mmoja mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea mkoani Ruvuma amejifungua watoto watano hai kwa wakati mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji wa uzazi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea.
Akizungumza Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Dkt.Benedict Ngaiza alimtaja mwanamke huyo aliyejifungua watoto hao watano kuwa ni Sophia Mgaya(28) ambaye ni mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea na kuwa hali za watoto hao zinaendelea vizuri pamoja na kuzaliwa chini ya umri wa kawaida wa kuzaliwa ambao ni miezi tisa.
Alisema kuwa mama huyo alipokuwa akihudhuria kliniki hospitalini hapo uchunguzi uliokuwa ukionyesha kuwa tumboni mwake kuna watoto wanne ambao walikuwa wakiendelea vizuri tumboni humo lakini mnamo Mei 24 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi alianza kusikia uchungu na kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa upasuaji na kukutwa akiwa na watoto watano hai tumboni mwake.
Dkt. Ngaiza alisema kuwa watoto watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike na wote wako hai na wamewekwa katika chumba maalumu kwa sababu wamezaliwa wakiwa na umri wa wiki thelathini na nne(miezi nane) na siyo miezi tisa kama ilivyo kawaida.
Aidha alisema kuwa watoto hao wamezaliwa wakiwa na uzito mdogo huku mwenye uzito mkubwa akiwa gramu 730 na mwenye uzito mdogo akiwa na gramu 430 na huo ukiwa ni uzazi wake wa pili huku mama mzazi wa mwanamke huyo aliwahi kujifungua watoto watatu na wote wako hai na mmoja ni mtoto wa kiume anasomo kidato cha sita katika shule ya wavulana ya Songea.
Alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kutokea katika hospitali hiyo kwa sababu kumekuwepo na matukio ya akina mama kujifungua watoto wawili au watatu na siyo zaidi ya idadi hiyo kama kama ilivyotokea kwa mama huyo
No comments:
Post a Comment