Pages

Thursday, October 25, 2012

 




Wazazi tuwe makini na wasichana wa kazi

JUKUMU la malezi kwa watoto katika familia linawahusu wazazi wote wawili. Tofauti na ilivyokuwa huko nyuma siku hizi wazazi wote wawili wanapaswa kutafuta kwa ajili ya kusaidia familia. Mabadiliko hayo yamekuja baada ya hali ya maisha kuwa ngumu na kila mtu kuona hakuna sababu ya mmoja kubaki nyumbani.

Kila mzazi ana taratibu zake katika suala zima la malezi katika familia. Ingawa sote tunafahamu kuwa hakuna mzazi anayetegemea kumpotosha mtoto wake hata siku moja.

Wazazi wamekua wakiishi kwa imani na wasichana wa kazi na kweli baadhi ya wasichana wamekuwa wazuri katika jukumu la kulea watoto pamoja na familia kwa ujumla. Wamekuwa ni msaada mkubwa katika familia husika na pengine kubeba majukukumu makubwa kuliko ilivyotegemewa.

Baadhi ya wasichana wa kazi wamekuwa wakijitolea kulea familia iliyoachwa pengine na wazazi wote wawili na kubaki kwa upendo tu kulea familia isiyo yake.

Katika msafara wa mamba na kenge hawakosi, baadhi ya wasichana wa kazi wamekuwa hawako kama ambavyo mtu yeyote angetegemea, wamekuwa si walezi wazuri wawapo na watoto majumbani.

Hasa muda ambao wazazi wanakuwa wako katika kazi zao hawajui nini kinaendelea nyuma yao.

Kutikana na hali hii, kama mzazi unapaswa kuwa mwangalifu unapotaka kuishi na msichana wa kazi. Wanawake wengi wamekuwa wakihofia ndoa zao tu wawapo na wasichana wa kazi na kusahau suala la watoto kwamba wanalelewa namna gani wao wawapo katika shughuli zao.

Husahau kabisa kuhusu jukumu la wao kuchunguza mienendo ya watoto kwa sababu wanafika jioni wamechoka kutokana na majukumu waliyonayo. Wanachojali ni watoto wamekula, wamevaa na ni wazima kiafya. Wanasahau kuwa karibu na watoto wao ili kujua nini kina wasibu.

Je, watoto wanampenda dada yao au wana mchukia? Au dada anawachukia watoto? Hivi ni vitu vidogo vidogo ninavyovizungumzia hapa lakini vinaweza kugharimu maisha ya watoto wetu huko mbeleni na usijue tatizo lilianzia wapi.

Mabinti watokapo vjijini kuja kufanya kazi mijini, huiga aina ya maisha ya mjini kwa sababu baadhi wanaamini kila kinachofanyika mjini ni kizuri wakati wowote. Nina mfano hai na ndio ulionivuta niandike kuhusu wasichana wa kazi.

Nilikuwa mgeni mahali fulani ambapo mimi niliongozana na bosi wa dada wa kazi, baada ya kufika kwake akamwambia msichana wake atafute mkanda mzuri wa kuangalia (CD).

Yule binti kwa kuwa alikuwa na shughuli nyingine anafanya akamtuma mtoto wa huyo bosi wake ambaye hushinda naye nyumbani akatafute. Lakini badala yake mtoto akaongoza kule kwenye CD inayomfurahisha zaidi bila dada kujua.

Nilishangazwa kuona mtoto analeta picha za ngono. Alifanya hivyo kwa kuwa picha hiyo ndio inayomvutia.

Alipoleta ile picha akasema; “hii ndio CD nzuri mama tuangalie hii ni nzuri sana mama.” Mama akabaki amepigwa na butwaa asijue la kufanya. Fikiria huyu mtoto ana miaka minne wewe kama mzazi unategemea msipokuwapo mchana kitu gani kinaendelea nyuma yenu?

Alipohojiwa binti akasema; “nimeazima kibandani ili niangalie.” Lakini kwanini aangalie na mtoto asiangalie mwenyewe hana la kujibu anabaki kuuma uma meno.

Wazazi uliyempa jukumu la kukulelea watoto hivi unadhani ni sahihi hali ya ugumu wa maisha ndio inayotufanya tushindwe kuwa karibu na watoto wetu mara turudipo nyumbani?

Mtoto anayengalia picha za iana hiyo ni mdogo sana, hivyo chochote anachokiona yeye kwake ni sahihi, hajui baya wala zuri.

Hili jambo unalibebaje kifuani kama mzazi na ni namna gani ulitatue ili mtoto akili yake ikae sawa kwa sababu msichana wa kazi hakuona kama ni tatizo kuangalia ile picha na mtoto. Licha ya kwamba umri wa dada huyu haukustahili kuangalia picha za aina hiyo.

Wazazi wapaswa sasa kutenga muda wa kufuatilia kwa ukaribu mambo yanayofanywa na wasichana wao wa kazi.

Kisa hiki kilinisikitisha sana na kujikuta nikitamanio kuwaasa wazazi kuwa karibu na binti zao ili kufahamu wanafanya nini pindi wanapokuwa kazini.

Kama hatutakuwa karibu na watoto wetu ni dhahiri kwamba tutawafanya wakose na maadili mema, kwani tumeshuhudia wazazi wengi ambao watoto wao wamekuwa wakipoteza mwilekeo kwa kukosa malezi bora ya mama na baba.

Toa Maoni yako kwa habari hii










No comments:

Post a Comment